Kupenda ni jambo muhimu katika maisha ya mwanadamu, kwa sababu
asilimia kubwa ya matendo ya mtu huongozwa na mapenzi. Miongoni mwetu
kuna watu wanapenda waume/wake zao, mali, watoto, magari vyakula,
vinywaji, michezo na pengine aina fulani ya maisha.
Baadhi yetu tuko tayari kupoteza maisha kama tutaachwa na wapenzi au
kukosa mambo tuliyoyapenda. Pamoja na kwamba moyo hupata maumivu pale
mazuri yanapokosekana, bado kuna ukweli juu ya madhara ya kujitakia
yanayoweza kuepukwa na mtu anayeumia kwa kiwango cha kukosa usinginzi,
kulia mara kwa mara kiasi cha kushindwa kufanya kazi zake kama kawaida.
Kupenda kwa kiwango cha kushindwa kujizuia na kuvumilia ni hatari
kwa afya ya mwanadamu, kwani uchunguzi unaonesha kuwa watu wengi
wanaosumbuliwa na ugonjwa wa vidonda vya tumbo, moyo na wale wenye
magonjwa yasiyoonekana kitalaamu pamoja na wanaokufa ghafla ni athari
za msongo wa mawazo utokanao na kukosa mazuri wanayohitaji katika
maisha yao.(Jiulize ni kipi kinachokutia simanzi moyoni mwako).
Kisaikolojia kuutesa moyo kwa sababu mpenzi wako kakukataa ni
matokeo ya kufikiri vibaya kwani ushahidi uliopo miongoni mwetu
unaonesha kuwa mapenzi si kitu cha kudumu kwa miaka mingi na anayesema
anaweza kupenda jambo moja milele kwa kiwango kilekile ni mtu
anayejiwekea mtengo utakaomnasa mwenyewe na kumtesa.
Watu wengi tunaowaona wakipagawa baada ya kupewa talaka na waume zao
au kuondolewa mambo fulani waliyokuwa wanayapenda ni wale
walioyachukulia mapenzi kama kitu cha kudumu kisichoweza kubadilika,
huku wakisahau ukweli kuwa wanayopenda kwa wakati huo hawakuzaliwa nayo
na wala hawakuyapenda kabla.
Licha ya kuwepo kwa umuhimu wa kujiaminisha katika kupenda kwa
msingi wa muda mrefu, mtu hatakiwi kukataa mabadiliko yanapotokea kwani
ni wazi kwamba tuliyopenda tulipokuwa watoto si yale tunayopenda sasa.
Hivyo ni jukumu la kila mtu anayetaka kuwa salama na maumivu ya moyo
ya kumkosa ampendaye ni kuwa tayari kubadilika kutoka kupenda kitu cha
awali mpaka kijacho, kuliko kung’ang’ania wazo moja na kujitesa nalo.
Historia ya mafanikio ya watu inaonesha kuwa waliokuwa tayari kuacha
walivyovipenda na kuanza mambo mapya ndiyo waliofanikiwa. Mwalimu
wangu na bosi wangu Eric Shigongo aliwahi kuniambia kuwa alilazimika
kuondoka nyumbani kwao Mwanza,akaacha aliowapenda/alivyovipenda kuja
Dar es Salaam kutafuta maisha, leo hii ni miongoni mwa waliopiga hatua.
Katika hali ya kawaida ni vigumu sana kuondoka miongoni mwa watu
uliowazoea, kuacha makazi yako na kuhamia mkoa mwingine, kuachana na
mpenzi wako mliyeahidiana mambo mengi, lakini mafanikio na usalama wa
maisha unataka mtu awe jasiri wa kupokea changamoto zinazohusu mapenzi.
Ikiwa umekaa na mwanaume kwa muda mrefu na ukabaini kuwa hana
mtazamo wa kimaendeleo, uwe tayari kukubali mabadiko ya kumwacha na
kuanza maisha mapya.
Msomaji wangu, unaumia kwa sababu mpenzi wako ameamua kuachana na
wewe na sasa unafikiria kujiua, hebu kaa chini ufikirie kabla ya kuwa
na huyo maisha yalikuwa hayaendi? Kama sivyo kinachokuumiza hasa ni
nini mpaka unashinda unalia na kuutesa moyo wako?
Tambua kuwa dunia ina vitu vingi sana vya kupenda, ambavyo vimeumbwa
kwa ajili ya mwanadamu, usipopenda hiki haina maana hakuna cha kukufaa
kipo na asipokupenda ndugu yako wapo marafiki watakaochukua nafasi ya
mapenzi moyoni mwako na maisha yatasonga mbele kwa mafanikio makubwa,
unachotakiwa ni kujiamini.
No comments:
Post a Comment