Kama
kuna mtu ambaye amekuwa akisoma makala zangu tangu nilipoanza kuandika
na amekuwa akipenda kufanikiwa kimaisha namuomba kwa unyenyekevu, asiwe
miongoni mwa watu ambao watakuwa na tabia zifuatzo kwani haweza
kufanikiwa kimaisha.
Hufikiri, kusema na kufanya yasiwezekana
Watu
wasioweza kufanikiwa hujaa fikra za kutofanikiwa na mara nyingi
hulalamikia sana matatizo yao. Wakati mwingine wasioweza kufanikiwa
hugeuza mambo mema na kuyafanya yaonekane mabaya, jua likiwaka
watalalamika joto, likipoa watalaumu baridi, watalaumu foleni za
barabarani, yaani kwao kila jambo wataligeuza na kulipa sababu mbaya.
Hata wanaposhindwa kutekeleza jambo hutoa sababu, yote ni kuzilinda
fikara zao za kutofanikiwa.
Tabia hii hukua mpaka kufikia hatua
wanapowatazama wenzao hudhani kuwa wanawasengenya, kuwafanyia mambo
mabaya, kuwasaliti, ilimradi tu ni kuwa kinyume na mambo mema. Watu wa
namna hii hata kama watasaidiwa namna gani hugeuza misaada hiyo kuwa ya
kujipendekeza na mara nyingi hupuuza wema haraka na kueneza mabaya ya
mtu. Lakini pamoja na yote kutokana na fikra zao kuwa za kushindwa watu
wa tabia hii hukata tamaa mapema, pale wanapofanya jambo na kuonekana
lina ugumu kidogo.
Hutenda kabla ya kufikiri
Tabia ya pili ya watu
wasioweza kufanikiwa kimaisha ni hii ya kutenda jambo kabla ya
kufikiria. Watu wa aina hii, kuwa wepesi sana kununua vitu barabarani
mara tu wanaposhawashiwa na macho au wauzaji. Utakuta mtu bila hata
kujiuliza faida za kitu hicho anaamua haraka kukipata. Ataamua kwa
haraka kuoa, kuolewa, kukubali kujiingiza katika mapenzi na hata kufanya
jambo lo lote bila kujiuliza atanufaika vipi?
Hupenda kuzungumza zaidi ya kusikiliza
Watu
ambao wako katika hatari ya kutofanikiwa ni wale ambao daima ni wazuri
katika kuzungumza kuliko kusikiliza. Wao huwa ni wajuajia wa kila kitu,
hawako tayari kupokea ushauri. Siku zote wanapokuwa kwenye makundi ya
watu pengine wajuzi zaidi yao wao huwa hodari kujenga hoja kutetea mambo
yao hata kama hayafai. Unaweza kumkuta mtu ni kiongozi wa ngazi za juu,
amefanya kosa na watu wote wameona kuwa kakosea lakini mhusika hujiona
si mikosaji.
Mtu anapokuwa muongeaji sana huwa mgumu kupokea ushauri
wa ye yote, anachoamua yeye hukifanya kwa imani kuwa kinafaa. Ukiwa mtu
mwenya tabia ya aina hii huwezi kufanikiwa kabisa katika maisha yako.
Watafiti wa masuala ya biashara ulimwengini waliwahi kushauri kuwa
mipango mizuri ya kibiashara hutoka kwa watu masikini, ambao walisema
hufikiri zaidi namna ya kujikomboa kuliko matajiri wanavyofikiri katika
kujiendeleza, hivyo wakasema kama mtu anataka kufanikiwa kibiashara
lazima asikilize mawazo ya masikini si kuwapuuza kwa kujiona ni bora
zaidi yao.
Hukata tamaa mapema
Watu wanaotaka kufanikiwa
huchukulia ushindwa kama hatua ya kuelekea kwenye mafanikio, lakini watu
wasioweza kufanikiwa wanapojaribu mara moja au mbili kuvuka kikwazo
fulani cha kimaisha na kushindwa hukata tamaa na kutotaka kujaribu tena
kusonga mbele. Wanye tabia ya kushindwa kimaisha hawako tayari kudumu na
jambo moja linaloonekana kushindikana kwao kwa muda mrefu. Akiona
mwanamke ambaye ni mkorofi kidogo, haraka hukimbilia kumwacha na
kutafuta mwingine, mara nyingi si watu wavumilivu.
Akijaribu biashara
ya vitumbua kwa wiki moja na akaona havinunuliwi, anaaza kupika
maadazi, wiki moja baadaye yuko kwenye mihogo, basi ilimradi ni
kuhangaika kusikokuwa na tija katika maisha. Ukitaka kuwa mmoja kati ya
watu wasiweza kufanikiwa kimaisha, basi jaribu kuishi maisha ya kukata
tamaa mapema unapofanya mambo.
Hujaribu kuwarudisha nyuma wengine
Wasioweza
kufanikiwa katika maisha huwa na tabia moja ya ajabu ambayo ilianzishwa
na Hawa mwanamke anayetajwa katika Kitabu cha Biblia kuwa ni mtu wa
kwanza kufanya dhambi. Mwanamke huyu alipodanganywa na nyoka na kuchuma
tunda hakutosheka na dhambi zake, bali alimpelekea na mumewe Adamu naye
akala. Mara nyingi watu walioshindwa kimaisha kuwa na tabia za
kuwashawishi watu wengine wawe kama wao katika mawazo na matendo.
Tabia
za watu wa aina hii huwa si za kimaendelezo kwa vile wao hudhani kuwa
njia zao ni sahihi na hivyo hujaribu kwa nguvu zao kuwarudisha wengine
nyuma ili wawe kama wao. Ni watu wenye wivu wa ‘kijinga’ wakiona
mwingine anaendelea katika hiki na kile humpiga vita ili afilisike. Ni
wingi wa fitina, uchonganishi. Wenye tabia za kutofanikiwa hudhani kuwa
kukwama kwao hutokana na vikwazo vinavyoletwa na wengine. “Kwa sababu
jamaa kanikwamisha hiki na kile, nimkwama kwa sababu ya kaka yangu”
Hupoteza muda mwingi
Watu
ambao hawawezi kufanikiwa ni wale ambao hupoteza muda mwingi kufanya
mambo yasiyokuwa na tija, kwa kuangalia Tv, kusengenya watu, kunywa
pombe, kufanya starehe na kutumia muda hovyo kwenye kazi ambazo hazina
msaada kwao. Wapo watu mahodari kutembelea kwenye nyumba za wengine na
kuongea huko kutwa nzima bila kujali kama muda waliopoteza wangeweza
kufanya kazi na kujipatia kipato.
Huchagua mambo rahisi
Wakati
mwingine mafanikio huhitaji kufanya kazi ngumu zenye kuchosha, lakini
watu wasiokuwa na uwezo wa kufanikiwa wanapoletewa mambo mawilii huwa
wepesi zaidi kuchagua jepesi kulifanya. Kama ni kazi, basi zisiwe ngumu
sana ziwe nyepesi nyepesi ambazo watazifanya bila jasho. Watu wasiokuwa
kwenye njia ya mafanikio hawapendi kujituma, wepesi kuchoka na mara
nyingi hupenda sana kufanya kazi kidogo na kulala sana.
Tabia za watu
wasioweza kufanikiwa huwa ni za kukwepa kuwajibika. Hata kama kuna mtu
anataka kumpatia kitu na akamwambia awahi kesho yake asubuhi, huchelewa
kwa vile hawezi kujihimu asubuhi na kuacha raha ya usingizi, wakati
mwingine hata akiambiwa asubiri mpaka muda fulani huwa hayuko tayari
kusubiri.
No comments:
Post a Comment